Leo June 19, 2018 Vichanga mapacha wa kike ambao wana siku tano wamefariki dunia baada ya kuungua wakiwa kwenye mashine maalum ya kuhifadhia watoto jijini Harare nchini Zimbabwe.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Taifa hilo walikuwa wamewekwa kwenye eneo hilo kwa lengo la kupata jotoridi kuipa afya ngozi iwe na hali ya kawaida lakini waliishia kuungua hadi kufa.
Mama wa watoto hao mapacha, Belinda Balalika amesema kuwa alibaini watoto wake wamefariki dunia kabla ya usiku wa manani alipotaka kuwachukua kwa ajili ya kuwanyonyesha.
Ripoti ya uchunguzi binafsi uliofanywa na gazeti la Standard ilibaini kuwa ‘beam’ ya mwanga iliwekwa juu ya watoto hao lakini joto lake halikurekebishwa vizuri hali iliyosababisha hitilafu na kuwachoma watoto hao.
Afisa Mtendaji Mkuu wa hospitali hiyo, Nyasha Masuka alikaririwa akieleza kuwa baada ya kufanya postmortem ilionesha watoto hao walikosa hewa na kuzidiwa na joto kali lililowachoma, ingawa alisisitiza kuwa uchunguzi zaidi utafanyika.