Kutoka makao makuu ya nchi 104.4 Dodoma leo February 19 unaambiwa baadhi ya wajumbe wamegoma kuendelea na mjadala huo baada ya baadhi yao kukosa nakala ya rasimu ya kanuni za bunge.
Kanuni za Bunge Maalum la katiba kwa mwaka 2014 zimetungwa chini ya kifungu cha 26 moja ili kulisaidia bunge hilo kufahamu namna litakavyoendesha shughuli zake ikiwemo kujadili utaratibu utakaowawezesha wajumbe kuwasilisha na kujadili na hatimaye kupitisha masharti ya rasimu ya katiba mpya.
Kukosekana kwa rasimu hiyo ya kanuni za bunge maalum leo kumesitisha kabisa ratiba ya kuanza kuwasilishwa kwa rasimu ya katiba mpya baada ya baadhi ya wajumbe kugomea kuendelea kwa mjadala huo kutokana na kutopatiwa nakala zake.
Wakiwasilisha hoja zao kwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo Pandu Andu baadhi ya wajumbe hao wamesema kitendo cha baadhi yao kutokuwa na rasimu ya kanuni,kutasababisha washindwe kuipitia na kuijadili kwa usahihi rasimu hiyo ya katiba mpya.
Hivyo Kutokana na hoja hizo Katibu wa Bunge Dr.Thomas Kashilila alisimama na kuomba muongozo wa wajumbe juu ya kuahirishwa kwa shughuli za bunge ili kila mjumbe aweze kupatiwa nakala ya rasimu ya kanuni.
Kufuatia hoja hizo Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo ilibidi aahirishe bunge kwa zaidi ya dakika 30 na baada ya wajumbe kurejea ndani ya bunge aliwataka wazipitie kanuni hizo hadi Februari 24 mwaka huu watakapoanza kuzijadili ili kupata kanuni halisi.