Leo June 21, 2018 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeruhusu Mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, Harbinder Seth kuongea na mke wake mahakamani baada ya kutokumuona kwa muda wa miezi mitatu.
Ruhusa hiyo imetolewa leo June 21 na Hakimu Mkuu Mkazi, Huruma Shaidi baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha ombi hilo kufuatia kutokuwa na kibali cha kumuona mumewe huyo gerezani.
Kabla ya kutolewa kwa ruhusa hiyo, wakili wa utetezi, John Chuma aliomba mshtakiwa aweze kuonana na mkewe ambaye hajaweza kumuona kwa kipindi cha miezi 3 sababu kipindi chote hicho alikuwa amefiwa na mama mkwe wake( mama wa mkewe).
“Mheshimia tunaomba mshtakiwa namba moja (Sethi) aweze kuongea na mke wake ikiwezekana hata kumkumbatia ili aweze kumpa pole ya kufiwa na mama yake kwa sababu bado hajapata kibali cha kuruhusiwa kwenda kumuona gerezani”
Akijibu ombi hilo Wakili wa serikali kutoka TAKUKURU, Leornad Swai, alidai, ” kwa sababu ni ombi anaomba kusalimiana na mkewe hapa mahakamani sina pingamizi lakini kwa magereza kuna taratibu zake na mkewe alizivuruga yeye mwenyewe”
Kufuatia majibu hayo, Hakimu Shahidi aliruhusu mshtakiwa kuongea na mkewe mahakamani hapo chini ya uangalizi wa askari magereza.
Kesi hiyo ambayo leo ilikuja kwa ajili ya kutajwa, upelelezi bado haujakamilika, imeahirishwa hadi July 5, mwaka huu.
Mbali na Seth mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni James Rugemalira ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka kumi na mawili ya uhujumu uchumi ,utakatishaji fedha na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya shilingi bilioni mia tatu.