Leo June 22, 2018 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea kusikiliza kesi inayowakabili Viongozi wa CHADEMA kwa sababu Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amefiwa na kaka yake.
Pia mahakama hiyo imeagiza mshtakiwa wa 5, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko kuhakikisha anafika mahakamani katika tarehe ijayo kinyume na hapo atachukuliwa hatua.
Katika kesi hiyo ya kufanya maandamano washtakiwa walitarajiwa kusomewa maelezo ya awali (Ph) mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Wakili wa serikali Mkuu, Faraja Nchimbi amedai kuwa kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya Ph, lakini mshtakiwa wa kwanza Mbowe na Matiko hawapo mahakamani.
Kutokana na hoja hiyo, Mdhamini wa Mbowe, Greyson Selastine ameiambia mahakama kuwa Mbowe amefiwa na Kaka yake wa tumbo moja na msiba umesafirishwa kwenda Moshi.
Pia mdhamini wa Matiko, Patrick John alisimama na kudai kuwa anaumwa yupo Dodoma na ameambiwa apumzike.
Hata hivyo, wakili Nchimbi alipinga taarifa ya mapumziko ya Matiko akidai nyaraka zilizowasilishwa ni batili.
Kutokana na hoja hizo, Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi June 25 ili washtakiwa wasomewe maelezo ya awali na kusikilizwa hadi June 29,2018.
Mbali na Mbowe, mwingine ni Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba John Mnyika.
Pia Katibu wa chama hicho Dk.Vicenti Mashinji, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na mbunge wa bunda, Esther Bulaya.
Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo kula njama, ambapo inadaiwa February 1 na 16, 2018, Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.
Wanadaiwa kuwa February 16,2018 katika barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni washtakiwa hao wakiwa na wenzao 12 ambao hawapo mahakamani walikiuka tamko la kuwataka kutawanyika la Afisa wa polisi SSP, Gerald Ngiichi kwa kugoma kutawanyika na kupelekea uvunjifu wa amani.
Inadaiwa kugoma huko kulipeĺekea hofu na hatimaye kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na majeruhi kwa askari wawili ambao ni H.7856 PC Fikiri na E.6976 CPL Rahim Msangi.