Leo June 29, 2018 Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Ilala (RCO), Davis Msangi ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa alibaini maneno yaliyotamkwa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ni ya jinai baada ya kumuangalia katika mtandao wa YouTube.
Msangi ameyaeleza hayo wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo amedai kuwa April 2017 hadi January 2018 alikuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Patrick Mwita, Msangi amedai kuwa July 4,2017 alikuwa ofisini kwake, nyakati za Saa 7:30 mchana akipitia simu yake katika mtandao wa YouTube ambapo aliona kichwa cha taarifa kilichoandikwa ‘Magufuli afungwe Break’.
Msangi amedai kuwa alifungua na kusikiliza maudhui ya ndani na kwamba yeye kama mlinzi wa amani aliona katika matamshi hayo kuna jinai.
Amebainisha kuwa maudhui yalikuwa ni maneno kuongewa kwa sauti na kwamba kilichomfanya aone kuna jinai ni Maneno yaliyoongelewa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana mambo ya hovyo hovyo anatakiwa afungwe Break.
Pia amedai bunge la Tanzania lingekuwa na meno angepigiwa kura ya kutokuwa na imani lakini bunge letu ni dhaifu.
Shahidi huyo ameieleza mahakamai hiyo kuwa baada ya kusikia maneno hayo alifanya jitihada ili kujua maneno hayo ni halisi ama yametengenezwa.
Alibainisha kuwa wakati anaichezesha hiyo sauti YouTube aliona picha ya mbunge wa jimbo la Kawe, Halima Mdee. Kesi imeahirishwa hadi July 11,2018 ambapo mashahidi wa upande wa mashtaka wataendelea kutoa ushahidi katika kesi hiyo.