Leo July 9,2018 Polisi Jamii wawili wa eneo la Mbezi Luis na dereva mmoja wamefikishwa Mahakamani Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kukutwa na meno ya Tembo yenye thamani ya Sh.Mil 239.5.
Wakili wa Serikali, Faraja Nguka amewataja washtakiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi, Ally Salum kuwa ni dereva mkazi wa Mbezi Luis, Kefas Mlenzi na Polisi Jamii, Juma Mtali na Greyson Muhapa wote wakati wa Mbezi Luis.
Wakili Nguka amedai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja June 28,2018 katika eneo la Mbezi Wilaya ya Ubungo kwa pamoja walikamatwa wakiwa na vipande 30 vya meno ya tembo vyenye thamani ya USD 105,000 sawa na Sh.Mil 239,505,000 bila ya kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama pori.
Baada ya kusomewa shtaka hilo washtakiwa hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu kesi hiyo mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza hadi Mahakama Kuu.
Upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi July 23,2018.