Raia wa Marekani mkazi wa jimbo la Michigan, Lione Lionel Rayford, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya kusafirisha zaidi ya Kilo 2 dawa za kulevya aina ya Heroine.
Mmarekani huyo ameshtakiwa chini ya kifungu cha sheria Namba 15 (1)(a) cha sheria ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya sheria Namba 15 ya mwaka 2017.
Inayosomeka pamoja na paragrafu 23 ya Jedwali la kwanza la sheria ya uhujumu uchumi, sura ya 200 marejeo ya 2002 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria Namba 3 ya 2016.
Akimsomea hati ya mashtaka, Wakili wa serikali Constantine Kakula amedai kuwa, mshtakiwa ametenda kosa hilo July 4, 2018 huko katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Wanjah Hamza inadaiwa, siku hiyo, mshtakiwa alikutwa akisafirisha dawa ya kulevya aina ya Heroine yenye uzito wa kilogramu 2.188.
Hata Hivyo, mshtakiwa hakutakiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa, mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za dawa za kulevya hadi mahakama Kuu au mpaka wapate kibali kutoka kwa DPP.
Kufuatia hayo, mahakama imeamuru mshtakiwa kurudishwa rumande hadi July 19, 2018
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika.