Leo July 10, 2018 viongozi wa Mashirika mbalimbali ya Umma wamekutana kujadili namna ambavyo mashirika hayo yanaweza kushiriki katika utekelezaji wa ajenda ya viwanda.
Muda mfupi baada ya kushiriki mjadala huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dr. Philip Mpango ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi amezungumza na vyombo vya habari na kusema kuwa mashirika bado yana nafasi kubwa ya kushiriki katika uchumi hivyo mashirika ya Umma ambayo hayapeleki gawio serikalini yatachukuliwa hatua.
“Bado ni mwanzo tu, tunaanza jitihada za kutafufua mashirika haya ili yaweze kuchangia ipasavyo katika uchumi wa taifa, mashirika ya umma ambayo hayaleti gawio serikalini huo ni mwisho, tunataka kuona kwamba pale ambapo serikali imewekeza kwa niaba ya watanzania basi watanzania wanapata kile ambacho wanatarajia” Waziri Mpango
“Nilisha muelekeza Msajili wa Hazina afanye uchambuzi upya wa mashirika yote ambayo serikali inahisi iwe ni kwa asilimia mia au chini ya hapo, wasioleta gawio tutayafuta lakini hatutaishia hapo tutawawajibisha viongozi wa mashirika hayo kwa kutotimiza wajibu” Waziri Mpango