Mkuu wa Mkoa wa DSM Paul Makonda leo July 12, 2018 amekabidhiwa Ofisi mbili za waalimu kati ya tano zinazojengwa na Ubalozi wa China nchini kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za Mkuu wa Mkoa katika kupatia ufumbuzi kero za Waalimu.
RC Makonda amesema ofisi hizo za kisasa zina chumba cha Mwalimu Mkuu, chumba cha Mwalimu Mkuu msaidizi, ofisi ya Mwalimu wa Taaluma, ofisi ya walimu wote, ukumbi wa mkutano, chumba cha mhasibu, karani, mapokezi,stoo,chumba cha kubadilishia nguo, chumba cha kuhifadhi vifaa vya michezo, mitihani pamoja na vyoo na bafu huku jengo likiwa na madirisha ya vioo, AC, TV Flat screen, Meza za kisasa, Makabati, Droo na viti vya kisasa.
Akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya jengo iliyofanyika shule ya sekondari Makumbusho RC Makonda amesema kukamilika kwa ofsisi hizo kutatoa fursa ya upatikanaji wa madarasa matano yaliyokuwa yakitumiwa na walimu kama ofisi ambapo kwa sasa yatarejeshwa kwa wanafunzi.
Aidha RC Makonda amesema kampeni ya ujenzi wa ofisi 402 za walimu ipo katika hatua nzuri na hivi karibuni atakabidhi ofisi 50 zilizokamilika kwaajili ya kuanza kutumika na walimu.
Hata hiyo RC Makonda amemshukuru Balozi wa China Bi. Wang Ke kwa kujenga ofisi hizo ndani ya muda mfupi na kusema hali hiyo itasaidia walimu kuwa na morali ya kazi na kusaidia ufaulu kuongezeka.