Leo July 26,2018 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepokea barua ya kufutwa kazi kwa aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa TAKUKURU, Godfrey Gugai kama kielelelezo cha 6 katika kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zisizolingana na kipato chake.
Kielelezo hicho kimepokelewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada kutupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi waliokuwa wanapinga kupokelewa kwa kielelezo hicho.
Katika pingamizi la Wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa amedai kielelezo hicho hakipaswi kupokelewa kwa sababu aliyekiwasilisha si mtu sahihi.
Akitoa uamuzi wa kupokea kielelezo hicho, Hakimu Simba amesema, kifungu cha 34(b)(1) walichotumia upande wa utetezi kuwasilisha pingamizi hilo hakiusiani kabisa na mazingira ya kesi hiyo.
Hakimu Simba amesema aliyewasilisha kielelezo hicho ni shahidi Ayoub Akida ambapo katika ushahidi wake amedai yeye ni Afisa Utumishi Mkuu wa TAKUKURU, ambaye ndie anahusika katika kutunza nyaraka za wafanyakazi ikiwemo barua hiyo ya kufutwa kazi.
Amesema sababu zilizowasilishwa katika pingamizi la upande wa uetezi za kutaka barua hiyo isipokelewe mahakamani kama kielelezo hazina msingi hivyo amezikataa na barua imepokelewa kama kielelezo Namba 6.
Baada ya kueleza hayo Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi August 6 na 13,2018 ili kuendelea na ushahidi.
Mbali na Gugai, washtakiwa wengine, ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali.
Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali za zaidi ya Sh.Bilioni 3.6 kinyume na kipato chake, ambapo anadaiwa ametenda kosa hilo kati ya January 2005 na December 2015.