Leo August 13, 2018 Viongozi 9 wa CHADEMA akiwamo Mwenyekiti, Freeman Mbowe wamewasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya kutaka kuomba kesi yao ya iahirishwe hadi Mahakama ya Rufani itakaposikiliza rufaa yao na kutoa uamuzi.
Pia wameomba kesi hiyo iahirishwe mpaka maombi yao ya kutaka kesi iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu isitishwe usikilizwaji wake.
Maombi hayo yamewasilishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri na Mawakili wa utetezi Jeremiah Mtobesya na Peter Kibatala.
Wakili wa Serikali Mkuu, Dk. Zainabu Mango ameieleza mahakama kuwa wamepewa hati ya maombi hayo namba10/2018 na kwamba wapo tayari kuwasilisha majibu kinzani leo na kuwapatia upande wa utetezi.
Wakili wa utetezi Mtobesya naye aliomba wapewe siku mbili ili waweze kuwasilisha majibu ya nyongeza kama watakuwa nayo.
Baada ya kusikiliza upande zote Hakimu Mashauri amesema maombi hayo yatasikilizwa August 21, 2018 na Kwa upande wa kesi ya msingi nayo pia itatajwa mahakamani tarehe hiyo hiyo.
Mbali na Mbowe washtakiwa wengine ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba John Mnyika, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na mbunge wa bunda, Esther Bulaya.
Wengine ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji.
Washtakiwa hao wamekata rufaa Mahakama ya Rufani wakipinga uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutupilia mbali maombi yao ya marejeo dhidi ya maamuzi madogo yaliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.