Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa kesi inayomkabili Mwanajeshi MT 109795 Private Ramadhan Mlaku (28) anayedaiwa kumua askari mwenzie, MT 79512 SGT Saimon Munyama inasubiliwa ripoti ya mtaalamu wa milipuko ili kukamilisha upelelezi.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa lakini upelelezi bado haujakamilika.
Mwita ameeleza kuwa bado wanasubiri ripoti ya mtaalamu wa milipuko ili kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo.
“Pia mawasiliano kidogo yamesumbua kuhusu baadhi ya vielelezo baina ya Jeshi la JWTZ na Polisi, hivyo tunaomba ahirisho,” ameeleza Mwita.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba ameutaka upande wa mashtaka kuharakisha mchakato huo ili hatma ya kesi ijulikane ambapo ameahirisha kesi hiyo hadi September 6,2018 kwa ajili ya kutajwa.
Inadaiwa mshtakiwa huyo ambaye ni Mwanajeshi wa Kambi ya Jeshi Makongo ametenda kosa la mauaji October, 30, 2017 akiwa Makao Mkuu ya JWTZ Upanga Ilala Dar es Salaam ambapo alimuua askari mwenzie MT 79512 SGT Munyama.
Mwanajeshi huyo anaendelea kusota lumande kwa kuwa kesi hiyo haina dhamana.