Leo September 12, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaapisha viongozi watatu aliowateua hivi karibuni.
Viongozi walioapishwa ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) Dkt. John Kiang’u Jingu, Balozi wa Tanzania nchini Uganda Dkt. Aziz Ponary Mlima na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) CP Diwani Athumani Msuya.
Rais Magufuli amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU CP Diwani Athumani Msuya kuongeza kasi ya kushughulikia tatizo la rushwa nchini kwa kuhakikisha wote wanaokabiliwa na tuhuma za kujihusisha na rushwa wanafikishwa mahakamani na sheria inachukua mkondo wake.
Rais Magufuli pia amemtaka CP Diwani kuungalia upya muundo wa TAKUKURU ili uweke bayana majukumu ya Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, na kuhakikisha watendaji wa taasisi hiyo wanaoonekana kutofanya kazi kwa tija na kujihusisha na vitendo vya rushwa wanachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuondolewa kazini na kufikishwa mahakamani.
“Nataka ukaisafishe TAKUKURU, kuna baadhi ya wafanyakazi wa TAKUKURU wanajihusisha na rushwa, kawaondoe, nataka kuona TAKUKURU inashughulikia rushwa kwelikweli hasa rushwa kubwakubwa, ukipita huko vijijini wananchi wanateseka sana, wananyanyaswa na kuna dhuluma nyingi sana, na tatizo kubwa ni rushwa” -Rais Magufuli.
BOSS MPYA TAKUKURU AFANDE DIWANI AMEAPISHWA NA RAIS MAGUFULI