Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko wakamatwe na kufikishwa mahakamani ili wajieleze kwanini wasifutiwe dhamana kwa kukiuka masharti.
Mapema leo mdhamini wa Mbowe, aliieleza mahakama kwamba Mbowe yupo nchini Dubai kwa ajili ya matibabu. Naye mdhamini wa Matiko ameeleza kuwa Matiko yupo katika ziara ya Kibunge nchini Burundi.
Amri hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya kutolewa kwa maombi kutoka kwa Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi akiomba mahakama itoe amri ya kukamatwa kwa washtakiwa hao kwa sababu ya kukiuka masharti ya dhamana.
Wakili Nchimbi amedai washtakiwa wamekiuka vifungu vya sheria namba 157 hadi 160 vya sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Kutokana na maombi hayo, Hakimu Mashauri amesema anaamuru mshtakiwa Mbowe na Matiko wakamatwe na kufikishwa mahakamani hapo ili kujieleza kwanini wasifutiwe dhamana zao.
Awali kabla ya amri hiyo Wakili Nchimbi, alihoji kwanini Mbowe na Matiko hawapo mahakamani.
Mdhamini wa Mbowe alisimama na kueieleza mahakama kwamba Mbowe yupo Dubai kwa ajili ya matibabu na hajawahi kusema kwamba yupo Afrika Kusini.
“Nimeongea naye moja kwa moja yupo nchini Dubai,“ameeleza.
Naye mdhamini wa Matiko alisimama na kuieleza mahakama kwamba Matiko amepata ziara ya Kibunge na yuko nchini Burundi, ambapo anawasilisha vielelezo ikiwemo tiketi ya ndege.
Licha ya kutokuwepo kwa washtakiwa hao, Nchimbi aliwasomea maelezo ya awali washtakiwa wengine 7 ambapo aliwakumbusha mashtaka yao lakini washtakiwa waligoma kukubari kama kweli ama lah hadi wapate uwakilishi kutoka kwa wakili wao Peter Kibatala ambaye hakuwepo mahakamani. Kesi imeahirishwa hadi November 12,2018.
Mbowe na viongozi wenzake 8 wa CHADEMA, wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 112 ya 2018.