Leo November 21, 2018 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa maagizo kwa upande wa mashtaka katika kesi ya kutoka lugha ya matusi inayomkabili Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kuhusu suala la upelelezi.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita alimueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kusikilizwa lakini shahidi Abdi Chembea hakufika kwa kuwa kesi ilipangwa kusikilizwa siku ya sikukuu.
Hakimu Simba amesema kuwa hawawezi kumlaumu shahidi kwa sababu kwa mujibu wa taratibu kesi inapopangwa siku ya mapumziko au sikukuu basi mshitakiwa anapaswa kufika siku inayofuata.
Kutokana na hatua hiyo, upande wa mashitaka umeiomba mahakama itoe hati ya wito kwa shahidi ili aweze kufika mahakamani kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.
Hakimu Simba ameahiriaha kesi hiyo hadi December 10 na 11, 2018 kwa ajili ya kusikilizwa ili hadi ifikapo mwishoni mwa mwaka iweze kuisha.
Mdee anadaiwa kutenda kosa hilo July 3, 2017 maeneo ya Ofisi za Chadema zilizopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, Dar es Salaam ambapo alimtukana Rais Dk John Magufuli kwamba “anaongea hovyohovyo anatakiwa afunge break”, kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.