Siku kadhaa zilizopita maeneo ya Mwananyamala aliokotwa mtu anaitwa Yusuf ambae wakazi wa eneo husika walidai kushuhudia mtu huyu akitelekezwa na gari la Wagonjwa la kitengo cha mifupa Muhimbili (MOI) ishu ambayo ilionekana ni ukatili.
Yani haijawahi kutokea kushuhudiwa kwa gari la mgonjwa likimtelekeza mgonjwa kwa makusudi sehemu ambayo hata haijui au hakuridhia kuachwa hapo, hayo ni maelezo ya wakazi wanaodai kushuhudia mgonjwa huyu akishushwa kwa lazima kutoka kwenye gari hilo la wagonjwa..
Mgonjwa Yusuf anasema alishushwa maeneo ya Mwananyamala bila yeye kuridhia na kwamba gari lililomshusha ni la wagonjwa kwenye kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI)
Baada ya hapo millardayo.com imefanikiwa kumpata afisa habari wa Moi Jumaa Almasi ambae amezungumzia lawama hizi kwa kuanza kusema >>> ‘Haijawahi kutokea tukaamua kumtelekeza mgonjwa sehemu yoyote ile bali kilichotokea ni kwamba Yusuf alilazwa kwenye wodi yetu toka mwaka jana ambapo ametibiwa na kupona ila hajatambuliwa na ndugu wala rafiki yeyote toka kipindi hicho alicholetwa mpaka sasa’
‘Wagonjwa wa aina hii tunao wengi, mtu anapata ajali analetwa hapa lakini kwa miezi anashindwa kutambuliwa na ndugu, mwishowe akishapona anabaki hapahapa, anakua anatoka nje asubuhi kuota jua kisha anarudi ndani jioni kitu ambacho kinakua kigumu kwetu sababu wodi haitoshi, ndio maana mtu akishapona tunamuuliza kwao wapi kisha tunampeleka ili kupisha nafasi ya kitanda wodini’
‘Yusuf aliulizwa kwao ni wapi akasema Mwananyamala hivyo gari letu kwa kuzingatia utaratibu ambao tunao siku zote likampeleka nyumbani manake alikua ameshapona, ni wagonjwa wengi tumekua tukiwapeleka makwao pindi wanapopona na kupata fahamu, nakumbuka kuna mmoja tulimpeleka mpaka Tanga lakini kwenye eneo alilotuelekeza kila mmoja akasema hamjui hivyo tukarudi nae Dar’
‘Sio hapa tu tuna wagonjwa wengine tunaowapeleka sehemu nyingi za Tanzania mtu anaweza kawa kasafiri anakuja kwa shughuli nyingine kabisa huku Dar es salaam kisha anapata ajali lakini anapokuwa sawa anatuambia mimi natoka Mwanza au Musoma, tunamsafirisha tunamsindikiza kwa gaharama za taasisi mpaka kule ambako yeye anasema anatoka’
‘Labda kuna kitu niwaambie Watanzania wagonjwa wa ajali ni wengi sana ambapo kwenye hii wodi inayotakiwa kuwa na wagonjwa 35 unakuta ina wagonjwa mpaka 70, sasa unapokuwa na wagonjwa wanaotakiwa kutoka wodini lakini wanaendelea kuwepo wodini tayari nafasi inakua finyu’
‘Kwa mfano sasa hivi sasa tuna wagonjwa 7 wanatakiwa waende nyumbani manake tiba wameshamaliza lakini wapo wodini wanaamka wanapewa chakula wanakula, wanatoka nje wanaota jua wanarudi siku zinaenda’
‘Tunaomba watanzania waelewe kuwa Yusuph hakutupwa kama inavyodaiwa isipokuwa ni kutokana na maelekezo yake na tumekua tukifatilia maelekezo yake kwa muda wa miezi 6 akiwa wodini akisema anatoka hapa anatoka hapa’ – Jumaa