Klabu ya Singida United imepangwa kucheza mechi ya ufunguzi dhidi ya Kaimu bingwa wa Ligi Kuu ya Kenya, Bandari FC, katika michuano ya SportPesa Cup inayotarajiwa kutimua vumbi kwa msimu wa tatu mfululizo kuanzia Januari 22-27 katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.
Ratiba hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu, iliwekwa hadharani na waandaaji wa michuano hiyo, kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa ambapo mabingwa mara 27 wa Tanzania Bara, klabu ya Yanga wataumana na mabingwa wa Ngao ya Jamii ya SportPesa, timu ya Kariobangi Sharks kutoka nchini Kenya majira ya saa 10:15 jioni katika mechi ya pili ya siku ya ufunguzi
Mabingwa watetezi Gor Mahia wataumana uso kwa uso na Mbao FC kutoka jijini Mwanza siku ya Januari 23 majira ya saa nane kamili mchana huku mtanange wa mwisho kwa hatua ya robo fainali ukipigwa kati ya Mabingwa wa Tanzania Bara, Simba SC watakaowavaa AFC Leopards majira ya saa 10:15 jioni.
Mkurugenzi wa Mashindano (TFF), Salum Madadi amesema maandalizi yote ya shindano yamekamilika, huku akiwataka mashabiki wa soka nchini kujitokeza kwa wingi uwanjani kushuhudia mechi kali na za kusisimua. “Mashindano ya mwaka huu sio ya kukosa kwa kila mpenzi wa soka nchini huku tukiwa na Imani kuwa timu zetu zitafanya vizuri na kubakisha Kombe nyumbani”>>> Salum Madadi
Bingwa wa mashindano atakutana uso kwa uso na timu ya Everton kutoka Ligi kuu ya Uingereza katika mechi ya kirafiki itakayopigwa nchi atakayotoka mshindi. Hii itakuwa ni mara ya pili kwa klabu ya Everton kuzuru Afrika Mashariki baada ya kufanya hivyo mwaka 2017 ambapo walicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Gor Mahia aliyekuwa bingwa kwa mwaka huo.
“Ratiba hii inatudhihirishia kuwa tutakuwa na wiki ya msisimko wa soka jijini Dar es Salaam. Nipende kutoa rai kwa mashabiki na wapenzi wa soka kuhudhuria uwanjani kwa wingi kuunga mkono maendeleo ya soka la ukanda huu,” >>>Tarimba Abbas Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti SportPesa Tanzania
Mpenja katangaza goli kabla ya kona kupigwa, ataomba kutotangaza game za timu yake