Tunayo story kuhusu Mahakama Kuu ya Tanzania kutupilia mbali pingamizi za Upande wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwenye kesi ya kikatiba inayopinga Wakurugenzi kusimamia Uchaguzi.
Uamuzi huo unatokana na Serikali kuwasilisha pingamizi kupitia hoja zao wakidai shauri hilo lilifunguliwa kinyume na sheria kutokana na kuwepo kwa mapungufu katika hati ya kiapo.
Pia katika hoja zao wamedai kuwa shauri hilo halikuwa na maana yoyote, hivyo inaomba mahakama isiipe kipaumbele.Katika maamuzi yake Jaji Gwala amesema anatupilia mbali pingamizi hizo za serikali.
Kutokana na maamuzi hayo ya Mahakama Kuu, shauri hilo linasubiri kupangiwa Majaji kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Katika kesi hiyo namba 6, mdai ni Bob Chacha Wangwe, anayewakilishwa na Wakili Fatuma Karume, anapinga Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Manispaa kuwa wasimizi wa uchaguzi kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Anadai kuwa hiyo ni kinyume cha Ibara ya 74 (14 ) ya Katiba ya Nchi ambayo inapiga marufuku kwa mtu yeyote anayehusika na uchaguzi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa na kwamba ana haki ya kupiga kura tu.