Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imesema inasubiri maamuzi ya Mahakama ya Rufani kuhusu dhamana ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko ndipo itapanga Hakimu mpya wa kusikiliza kesi yao ya uchochezi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina alisema kuwa katika kesi hiyo bado hawajampangia Hakimu yoyote mpaka watakapopata majalada ya maamuzi kutoka Mahakama ya Rufaa.
Awali, Wakili wa Serikali, Ester Martin alidai kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba wanasubiri maamuzi ya Mahakama ya Rufaa.
Wakili wa Utetezi, Profesa Abdallah Safari alidai hawana pingamizi na kwamba rufani iliyokatwa na upande wa mashtaka Mahakama ya Rufaa itasikilizwa Februari 18, 2019.
Hakimu Mhina aliahirisha kesi hiyo hadi February 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Novemba 23, 2018 Jaji Wilbard Mashauri akiwa Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, alifuta dhamana kwa Mbowe na Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana.
Baada ya maamuzi hayo, washtakiwa hao wakiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala walikata rufaa Mahakama Kuu kupinga maamuzi ya mahakama hiyo ya kufuta dhamana.
Hata hivyo, baada ya mahakama Kuu chini ya Jaji Sam Rumanyika kusikiliza mapingamizi ya pande zote iliamua kuanza usikilizaji wa rufaa hiyo.
Upande wa serikali ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi ulidai kuwa wamekata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga maamuzi yaliyotolewa na kuiomba mahakama hiyo kuacha kuendelea kusikiliza rufaa hiyo kwa sababu haina mamlaka.
Hata hivyo, baada ya upande wa serikali kuwasilisha rufaa yao, kuliibuka malumbano ya kisheria baina ya mawakili wa pande zote, huku mawakili wa kina Mbowe wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala, walipinga uhalali wa taarifa ya serikali ya kusudio la kukata rufaa kwa madai hawajafahamishwa na Msajili wa Mahakama Kuu kuhusu kuwepo kwa taarifa hiyo.
Mbali na Mbowe na Matiko, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu ambao wote walikuwepo mahakamani.
Katika kesi ya msingi, washitakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka 2018 maeneo ya Dar es Salaam.
ALIEJENGA NYUMBA MPAKANI MWA KENYA NA TANZANIA “SIJUI MIMI RAI WA WAPI”