Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema haina mamlaka ya kumfutia kesi wala kumpa dhamana aliyekuwa Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura.
Wambura alifikishwa mahakamani hapo February 11, 2019 akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kusomewa mashtaka 17 ikiwemo utakatishaji fedha wa Mil.75.
Hatua ya mahakama kueleza hayo inatokana na maombi yaliyowasilishwa na Wakili anayemtetea Wambura, Majura Magafu ambapo aliiomba mahakama kumfutia mashitaka mteja wake kwa madai hati ya mashitaka si ya uhujumu uchumi.
Katika uamuzi wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina amesema kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Amesema amesikiliza hoja za Wakili Magafu lakini amefungwa mikono kutokana na Mahakama hiyo kutopewa mamlaka ya kusikiliza kesi za namna hiyo labda kitolewe kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
“Hii mahakama haina mamlaka ya kuifuta hii kesi, pia suala la kama hati ya mashitaka kuwa sahihi ama si sahihi nayo mahakama hii haina mamlaka,”amesema.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mhina amesema rufaa ipo wazi, pia mshitakiwa ataendelea kubaki rumande kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kumpa dhamana.Kesi imeahirishwa hadi February 28, 2019.
Katika kesi hiyo mshtakiwa wambura anakabiliwa na shtaka moja la kughushi, Shtaka moja la kutoa nyaraka za uongo, mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha.
Katika shtaka la 3 hadi la 15 mshtakiwa anadaiwa kujipatia kiasi jumla ya zaidi ya Sh.Milioni 95
kwa njia ya udanganyifu akidai kuwa fedha hizo ni sehemu ya malipo ya jumla ya kiasi cha fedha mbali mbali na riba kutoka kwa Jek huku akijua kuwa siyo kweli.
Katika moja ya mashtaka hayo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu imedaiwa, Juni 17.2015 huko katika ofisi za TFF kwa njia ya udanganyifu, Wambura alijipayia sh. Milioni 10 kutoka TFF kwa kuonesha kuwa ni malipo ya USD 30,000 pamoja na riba kutoka kwenye kampuni hiyo ha Jeck jambo ambalo siyo kweli.
Katika mashtaka ya utakatishaji fedha imedaiwa, kati ya Agosti 15 na Oktoba 21 huko katika ofisi za TFF mshtakiwa alijipatia sh. Milioni 25,050,000 kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.
ALIEJENGA NYUMBA MPAKANI MWA KENYA NA TANZANIA “SIJUI MIMI RAI WA WAPI”