Huduma ya kuhamia mtandao mwingine bila kubadili namba ya simu ya kiganjani au MNP, ambacho ni kifupisho cha Mobile Number Portability, ina maana kuwa mtumiaji anabaki na namba yake ya awali iwapo ataamua kuhamia mtandao mwingine wa simu za kiganjani nchini Tanzania. Kimsingi, ni huduma ambayo inakuwezesha kubakia na namba yako ila kujali unatumia mtandao gani.
Hivyo, iwapo utabadilisha mtoa huduma wa simu za kiganjani hutakuwa na haja ya kusumbuka kuwataarifu watu wako wa karibu – marafiki, familia na wafanyakazi wenzako au washirika wako
kwamba umebadilisha namba kwani inabakia ileile.
Faida za huduma hii kwa mtumiaji ni kama ifuatavyo:
1. Ataendelea kutumia namba yake ya awali anapohama kutoka mtoa huduma mmoja kwenda
mwingine na hivyo kufurahia uhuru na utulivu katika matumizi.
2. Atapokea simu na meseji bila kujali ni mtandao upi amehamia na bila kuwa na haja ya kuwataarifu marafiki, familia na wafanyakazi wenzake au washiriki wake kwamba amebadilisha mtoa huduma wake.
3. Ataokoa fedha kwa kuwa hatakuwa na haja ya kununua laini mpya kwa kila mtoa huduma au kuwa na simu ya kiganjani zaidi ya moja.
4. Ataweza kuchagua mtoa huduma ambaye anaona anatoa huduma bora zaidi, anakidhi matarajio
yake na ana ubunifu katika kutoa huduma.