Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA imewafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi watu wawili akiwemo mtalaamu wa IT raia wa Kenya Brian Lusiliola kwa tuhuma za makosa sita ya uhujumu uchumi ikiwemo kuisababishia serikali hasara ya Mil.64. Mbali na Lusiliola washitakiwa wengine ni Ahmed Ngassa na Kampuni ya Inventure Mobile Tanzania Ltd.
Washitakiwa hao wamesomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali Jackline Nyantori mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi, inadaiwa kuwa katika makosa hayo sita yapo ya kuingiza, kutumia na kusimika vifaa vya mawasiliano bila kuwa na leseni pamoja na kuisababishia serikali hasara.
Katika kosa la kuingiza vifaa nchini wanadaiwa kutenda kati ya tarehe tofauti kati ya Januari 1 na Desemba 31, 2018 wakiwa katika jengo la Tanzanite Kinondoni ambapo kinyume na sheria waliingiza nchini vifaa vya mawasiliano aina ya Proliant
Kosa la kusimika vifaa wanadaiwa kulitenda kati ya tarehe tofauti kati ya Januari 1 na Desemba 31, 2018 wakiwa jengo la Tanzanite walisimika vifaa vya mawasiliano vya Kielektroniki kinyume sheria.
Pia wanadaiwa kutumia vifaa hivyo kati ya Januari 2 na Machi 11,2019 kinyume na sheria ambapo wanadaiwa kuendesha vifaa vya mawasiliano ya simu za Kimataifa bila kuwa na leseni.
Pia wanadaiwa kumiliki vifaa kilaghai na kutumia bila kuthibitishwa ambapo inadaiwa walitenda Januari 2 na Machi 11, 2019 katika jengo la Tanzanite Park ambapo kinyume na sheria walilaghai na kutumia vifaa hivyo visivyothibitishwa.
Katika kosa la mwisho wanaidaiwa kuisababishia serikali hasara ya Mil.64 ambapo wanadaiwa kulitenda kati ya Januari 2 na Machi 11, 2019 katika jengo la Tanzanite Park ambapo wanadaiwa walisababishia hasara hiyo.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote na wamerudishwa mahabusu kwa sababu ni kesi ya Uhujumu Uchumi ambapo Wakili Nyantori alidai upelelezi haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Aprili 3, 2019.