STRAIKA wa Simba raia wa Burundi, Amissi Tambwe ameweka rekodi nyingine ya pekee ya kufunga mabao 19 katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa staili ya aina yake.
Katika mabao hayo mchezaji huyo hajapachika bao hata moja kwa shuti kali.
Tathmini ya kiufundi inaonyesha kuwa fowadi huyo hajapachika bao lolote kati ya hayo kwa shuti la nje ya 18 na hata aliyoyafungia ndani ya 18 ni ya kuminya tu na kumchambua kipa kisha kumalizia nyavuni.
Rekodi hiyo aliyoiweka alitumia vyema pasi za viungo washambuliaji wa timu hiyo, Ramadhani Singano ‘Messi’, Haroun Chanongo na Amri Kiemba huku akicheza kijanja na huku akiutumia udhaifu wa mabeki wa Tanzania.
Katika historia ya washambuliaji, wengi wanafunga mabao kwa mashuti ndani na nje ya 18, lakini kwa Tambwe ni tofauti yeye anafunga kwa kutumia akili nyingi katika kumchambua kipa golini akiwa katika eneo zuri la kufunga.
“Nina uwezo wa kufunga mabao kwa kupiga mashuti, lakini nimeshindwa kufunga kutokana na kutopata nafasi ya ndani au nje ya 18 kufunga kwa mashuti.
“Hiyo imetokana na mfumo wanaoutumia makocha wetu, mara nyingi wanataka nicheze nikiwa ndani ya 18 na si nje kama wanavyocheza washambuliaji wengine, ndiyo maana muda wote unaniona nikiwa uwanjani nasimama katika eneo hilo, kama mshambuliaji unatakiwa muda wote ucheze karibu na goli la timu pinzani,”alisema Tambwe.
SOURCE: MWANASPOTI