BEKI na nahodha wa Yanga Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amefichua siri kwamba alikuwa katika wakati mgumu katikati ya msimu huu ambapo ilikuwa kidogo aachane na soka.
Akizungumza na Mwanaspoti Cannavaro alisema baada ya sare ya mabao 3-3 dhidi ya Simba alianza kupata wakati mgumu katika kikosi hicho ambapo alianza kuzushiwa mambo mengi likiwemo suala la kuwa ameshuka kiwango.
Cannavaro alisema kauli hizo zilimfanya kuishi kwa kukosa raha ambapo kila muda ulipokuwa ikienda ndipo mengi yalizidi kuibuka ambapo alipata taarifa kuwa alikuwa aachwe katika usajili wa dirisha dogo.
Alisema wakati akiwa katika kambi ya maandalizi ya mzunguko wa pili nchini Uturuki alifikiria kwa kina na aliona ni vyema akaachana na soka lakini wakati akijiandaa kuandika barua alipata ushauri kutoka kwa mmoja wa viongozi wa klabu hiyo Salum Rupia na kufuta uamuzi wake.
“Nilikuwa katika wakati mgumu sana nakumbuka kuna mechi moja tukiwa Uturuki kocha (Hans Pluijm) alitaka niingie, nicheze lakini sikuweza kucheza kutokana na kusongwa na mawazo, nilishajiandaa kuandika barua kwa uongozi kuwaomba waniache niache kucheza soka,” alisema Cannavaro.
“Unajua kikubwa ni maneno kuwa mimi nimeisha sina jipya, naisababishia timu kufanya vibaya, sikuona kama nahitajika tena kwenye timu huku wengine wakiniambia Yanga wana mpango wa kuniacha katika usajili, lakini nashukuru nilimfuata Rupia wakati nikimtaarifu kuwa nakusudia kuacha soka akanikataza na kunipa moyo wa kupambana,”alisema.
Rupia alikiri hali hiyo kutokea na alisema alilazimika kutumia muda mwingi kumshauri beki huyo ambaye kwa sasa ni nguzo muhimu katika safu ya ulinzi.
SOURCE; MWANASPOTI