Leo July 25, 2019 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesafiri kwa treni ya TAZARA kutoka Jijini DSM kuelekea Kisaki Mkoani Morogoro na baadaye atakwenda Rufiji Mkoani Pwani ambako kesho atakuwa Mgeni Rasmi katika sherehe ya kuweka jiwe la msingi mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji.
Kabla ya kupanda treni, Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amezungumza na viongozi wa TAZARA na kuwataka kuwasilisha mapendekezo yao juu ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuboresha usafirishaji wa mizigo na abiria kupitia TAZARA.
Rais Magufuli amesema Serikali inatambua umuhimu wa TAZARA na haiwezi kuiacha ikifanya kazi kwa ufanisi mdogo usiowaleta manufaa Watanzania kama ilivyokusudiwa.
TAZARA iliyojengwa kwa msaada kutoka China, ilianza kutoa huduma mwaka 1975 na inamilikiwa kwa ubia wa asilimia 50 kwa 50 wa nchi ya Tanzania na Zambia.
Reli ya TAZARA yenye urefu wa kilometa 1,860 ina uwezo wa kusafirisha tani Milioni 5 za mizigo kwa mwaka lakini kutokana na uwekezaji mdogo uliosababisha upungufu mkubwa wa injini na mabehewa inasafirisha chini ya tani laki 3 kwa mwaka.
Mkurugenzi Mkuu wa TAZARA Bw. Bruno Chingandu na Meneja Mkuu wa TAZARA Tanzania Fuad Abdallah wamemueleza Rais Magufuli kuwa tayari mapendekezo ya mabadiliko ya sheria yamewasilishwa Serikalini ili kuwezesha kila nchi kuwekeza katika TAZARA kwa lengo la kuboresha usafirishaji wa abiria na mizigo.
Rais Magufuli ameagiza mchakato wa kufanya marekebisho ya sheria hiyo uharakishwe ili juhudi za kununua injini na mabehewa zifanyike haraka.