Vigogo wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) wameangua vilio vya furaha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kuachiwa huru.
Hatua ya kuachiwa huru kwa vigogo hao akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, James Mataragio ni baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kutokuwa na nia ya kuendelea na mashitaka dhidi yao.
Mataragio ambaye hakuwepo mahakamani, alirejeshwa katika nafasi yake ya kazi hivi karibuni baada ya agizo la Rais John Magufuli.
Washtakiwa wengine walioachiwa huru ni katika ni George Seni, aliyekuwa Kaimu Meneja wa Uvumbuzi; Welington Hudson, aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Utawala; Kelvin Komba, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mkondo wa Juu na Edwin Riwa , aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mipango.
Kwa pamoja washitakiwa hao wameachiwa huru mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kupitia Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon kuomba kuiondoa kesi hiyo tangu Julai 10, 2019.
DPP kwa niaba ya Jamuhuri amesema hakusudii kuendelea kuwashtaki washtakiwa hao katika kesi hiyo na akaomba iondolewe chini ya kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA) Sura ya 20.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mhina aliwaachia huru washitakiwa hao chini ya sheria hiyo.
Wakiwa wanatoka mahakamani vigogo hao walianza kuangua vilio vya furaha.
Katika mashitaka yao Vigogo hao wanadaiwa kati ya Aprili 8, 2015 na Juni 3, 2016, wakiwa watumishi wa umma na waajiriwa wa TPDC kwa nafasi zao, wakati wakitimiza majukumu yao kwa makusudi walitumia madaraka vibaya.
Pia wanadaiwa walibadilisha na kupitisha bajeti na mpango wa ununuzi wa mwaka 2014/2015 na 2015/2016 kwa kuingiza ununuzi wa kifaa cha utafiti cha Airborne Gravity Gradiometer Survey, katika ziwa Tanganyika bila ya kupata kibali cha bodi ya wakurugenzi ya shirika hilo.
Inadaiwa kwa kufanya hicho, walikiuka kifungu cha 49(2) cha sheria ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 huku ikidaiwa kwamba lengo lilikuwa ni kujipatia manufaa yasiyo halali ya Dola 3.2 milioni ambazo ni sawa na Sh.Bilioni 7.2.