Mwandishi wa Habari za Kiuchunguzi, Erick Kabendera ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa madaktari wa Gereza la Segerea walimpima damu na kumchoma Sindano tatu kutokana na kushindwa kupumua.
Kabendera anayekabiliwa na kosa la utakatishaji fedha, amedai kuwa anapata maumivu makali katika mguu wa kulia na mfupa wa paja hivyo, anashindwa kutembea na kusababisha kuburuza mguu.
Kabendera ameyaeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile baada ya kutakiwa kueleza kama madaktari wamempatia tiba yoyote.
Amedai kuwa madaktari hao hawana vifaa vya kuwasaidia kugundua tatizo alilonalo hivyo, wamemshauri kufanya mazoezi.
Alidai mguu wa kulia na mfupa wa paja wa mguu huo una maumivu makali
“Nilifanya jitihada za kuzungumza na madaktari na niliomba dawa za kutuliza maumivu kwa sababu sipati usingizi. Madaktari waliahidi kuendelea kuniangalia,” amedai Kabendera.
Huku akionekana kuwa na maumivu makali, alidai alionana na daktari Alhamis iliyopita na juzi (jana) alimuona lakini hakumfanyia vipimo kwa sababu walikuwa na wageni hivyo, aliahidi kuonana naye leo.
“Nipo Segerea na kuna utaratibu wa madaktari kufanya matibabu kwa wagonjwa kila siku,” alidai.
Hatua ya Kabendera kueleza hayo ni baada ya Wakili wake, Jebra Kambole kudai kuwa hali ya mshitakiwa huyo inazidi kutetereka kwa sababu anashindwa kutembea vizuri na kushindwa kupumua.
Kambole amedai bado Kabendera hajafanyiwa matibabu vizuri kujua tatizo linalomsumbua na kuomba mahakama ielekeze magereza wampeleke hospitali yoyote ya Serikali ikiwamo Muhimbili ili wapate ripoti ya ugonjwa unaomsumbua.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai amewasiliana na Mkuu wa Gereza na kumueleza kuwa Kabendera anapatiwa matibabu na madaktari wamekuwa wakimuangalia mara kwa mara.
Amedai magereza wana utaratibu wao endapo wataona ugonjwa unaomsumbua unahitaji rufaa, watampeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Rwizile ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 18, mwaka huu 2019 na kumuelekeza Kabendera kuonana na daktari kisha itakapotajwa tarehe nyingine ataieleza mahakama kama amepata matibabu au la ili mahakama itoe maelekezo.
Kabendera ambaye rumande kutokana na kesi yake kutokuwa na dhamana hadi Mahakama Kuu, alifikishwa Mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, Agosti 5, 2019 akikabiliwa na mshtaka matatu, ambayo ni kuongoza genge la Uhalifu, kukwepa kodi na kutakatisha zaidi ya Sh. 173.2Milioni.