Mfanyabiashara Yusufu Ali maarufu ‘Mpemba wa Magufuli’ na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wamemuandika barua Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kuomba kukiri mashitaka hayo.
Katika kesi hiyo, mbali ya Mpemba washitakiwa wengine ni Charles Mrutu, Benedict Kungwa, Jumanne Chima, Ahmed Nyagongo na Pius Kulagwa.
Wakili wa Serikali, Elizabeth Mkunde amemueleza dai Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kwamba washitakiwa wameshaandika barua hivyo, anaomba mahakama iwape muda kwa ajili ya kuingia katika makubaliano.
Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 16, mwaka huu 2019 kwa ajili ya kutajwa.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka manne ya kujihusisha na biashara ya Meno Tembo yenye thamani ya Sh. Mili 785.6
Pia inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2014 na Oktoba, mwaka huu wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za serikali ambazo ni vipande vya Meno ya Tembo 50 vyenye thamani ya Dola za Marekani 180,000 sawa na Sh.Mili 392.8 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Pia inadaiwa Oktoba 26, mwaka huu, washitakiwa hao wakiwa Mbagala Zakhem, walikutwa na vipande vya meno ya tembo10 vyenye uzito wa kilo 13.85 vya thamani ya Dola za Marekani 30,000 sawa na Sh milioni 65.4.
Pia wanadaiwa Oktoba 29, mwaka huu walikutwa na vipande 36 vya Meno ya Tembo vikiwa na thamani ya Sh.Mil 294.6 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.