Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amepokea mapendekezo ya wataalamu wa mifugo wastaafu na wadau wa sekta ya binafsi yaliyotolewa ili kuboresha zaidi sekta ya mifugo nchini.
Akipokea mapendekezo hayo Prof. Gabriel amesema wizara itatumia taratibu mbalimbali kuhakikisha mapendekezo yaliyotolewa na wastaafu hao na wadau wa sekta binafsi yanafanyiwa kazi na kwamba wizara pia inafanya kila jitihada kuhakikisha afya ya watanzania inaimarika kwa kutumia mazao ya mifugo ikiwemo nyama na maziwa kutoka kwenye mifugo isiyo na magonjwa.
Prof. Gabriel amefafanua kuwa Asilimia 60 ya magonjwa ya binadamu yanasababishwa na mifugo hivyo wizara itahakikisha inadhibiti magonjwa ya mifugo pamoja na kuhakikisha inasimamia vyema soko la mifugo nje ya nchi.