Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu DSM, imeelezwa kuwa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ameshapona ila anashindwa kurudi nchini kwa kile alichokidai ni kuhofia usalama wake.
Hayo yameelezwa mahakamani hapo na mdhamini wake Ibrahim Ahmed, wakati wa kutajwa kwa kesi inayomkabili Mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki Tundu Lissu pamoja na wenzake watatu kuhusiana na makosa ya uchochezi.
Mwanzoni mwa mwezi Oktoba, 2019 Mwanasheria huyo wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alitangaza huenda akarejea nchini Septemba 07, 2019, lakini baadaye alisogeza mbele kwa kile alichokidai mpaka atakapohakikishiwa tena usalama wake.
Kesi hiyo ya uchochezi inayomkabili Tundu Lissu, inasimamiwa na Hakimu Thomas Simba, ambapo washtakiwa wengine ni Mhariri wa Gazeti la Mawio Simon Mkina, Jabir Idrisa, ambao wanashtakiwa kwa kosa la kuchapisha habari kinyume na sheria za huduma za vyombo vya habari.