Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu wawili akiwemo mchezaji wa zamani wa Timu za Mbeya City na Kagera Sugar, Deogratius Juliu (27) kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya aina ya ‘Heroine’.
Akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Ulrich Matei amesema Julius alinaswa Novemba 20 mwaka huu katika eneo la Mafiati Jijini Mbeya akiwa na Kete 27.
Amesema baada ya kumhoji alisema dawa hizo sio zake bali ni za rafiki yake ajulikanaye kwa jina la Kelvin Mwankuga (28) mkazi wa Mwakibete Jijini humo na kwamba msako ulianza wa kumtafuta na akanaswa kesho yake.
Kamanda Matei amesema watuhumiwa wapo selo na taratibu za kuwafikisha mahakamani zitaendelea baada ya uchunguzi kukamilika.
Hata hivyo Jeshi la Polisi Kitengo cha Dawati la Jinsia limezindua Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambapo, Mkuu wa Dawati hilo, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Janeth Masangano amesema wataendesha kampeni kupitia vyombo vya habari, mikutano ya hadhara pamoja na taasisi za dini.