Jeshi la Iran hatimaye limekiri kudungua “kimakosa” ndege ya abiria Ukraine siku ya Jumatano, runinga ya taifa ya Iran imeripoti.
Taarifa ya Jeshi inaeleza kuwa mkasa huo umetokana na “makosa ya kibinadamu” baada ndege hiyo kupita karibu na eneo nyeti linalomilikiwa na Kikosi cha Mapinduzi (Revolutionary Guards).
Maafisa waliofanya kosa hilo wataadhibiwa, taarifa hiyo imeeleza. Watu wote 176 ndani ya ndege hiyo wamepoteza maisha.
Hata hivyo nchi hiyo ilikabwa koo baada ya Marekani na Canada kudai kuwa taarifa za kijasusi walizonazo zinaonesha kuwa Iran iliidondosha ndege hiyo kwa bahati mbaya na moja ya makombora yake.
Kuanguka kwa ndege hiyo kulitokea saa chache baada ya Iran kushambulia kambi za kijeshi za Marekani nchini Iraq kwa makombora ya masafa marefu.