Mvua zinazoendelea kunyesha katika Mkoa wa Rukwa zimeendelea kusababisha maafa baada ya kusomba madaraja manne katika barabara ya Kasansa – Kilyamatundu inayounganisha Mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi iliyopo bonde la Ziwa Rukwa Wilayani Sumbawanga huku ikisababisha vifo vya watu watatu katika Wilaya ya Kalambo na Nkasi mkoani humo.
Mvua hizo zilizosomba madaraja katika Vijiji vya Muze, Kifinga, Lwanji na Msia vilivyopo Wilaya ya Sumbawanga imesababisha kukatika kwa mawasiliano baina ya kata na kata, Kijiji na Kijiji pamoja na Mikoa hali iliyoleta taharuki kwa wananchi wanaoishi katika bonde hilo lenye kata 13 na wakulima wengi wa mpunga wanaosafirisha bidhaa zao katika mikoa ya jirani.
Aidha, Mvua hizo zimesababisha vifo vya Mama mjamzito na mwanawe kwa kusombwa na maji ya Mto Kalambo huko Wilayani Kalambo na kifo cha mwanafuzi wa darasa la 4 mwenye umri wa miaka 12 katika Wilaya ya Nkasi ambae pia alisombwa na maji wakati akitoka shuleni kurudi nyumbani.
Hayo yamesemwa na RC Rukwa Joachim Wangabo alipofanya ziara ya kutembelea maeneo yaliyokumbwa na maafa hayo na hivyo kuwatahadharisha wananchi kuacha tabia ya kulazimisha kupita katika njia ya maji pindi wanapoona mvua ni kubwa na hivyo kuwataka kusubiri mvua ipungue ndipo waendelee na shughuli zao.