Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeagiza kukamatwa na kushtakiwa Watendaji wa Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO), Watendaji Wakuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Viongozi wa Kampuni ya Taifa ya Uwekezaji (NICOL) kutokana na kashfa ya wizi wa Tsh. bilioni 15.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mahmoud Mgimwa, amesema wamebaini watendaji wa NARCO na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi waliohudumu katika kipindi cha kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2015, walishirikiana kwa pamoja na Kampuni ya NICOL kuwaibia Watanzania fedha hizo.
Amehoji, iweje tangu mwaka 2008 ufisadi huo umefanyika bila wahusika kuchukulia hatua wahusika hao, hivyo akaitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwatafuta na kuwafikisha kwenye Vyombo vya Sheria.
Kamati hiyo imepongeza Uamuzi wa Serikali kuvunja Mkataba wa Mauzo ya Mali za Machinjio hayo baina ya Serikali na Kampuni ya NICOLl na kuyarejesha machinjio chini ya umiliki wa Serikali na kuitaka kufanya haraka kurejesha masoko ya nyama katika nchi za Falme za Kiarabu yaliyopotea kutokana na Usimamizi Mbovu wa waendeshaji hao wa zamani.
Waziri Mpina, ameihakikishia Kamati hiyo kuwa wote waliohusika na wizi na ubadhirifu hawatapona kwa kuwa Serikali inajua kuwa mbali na fedha hizo zilizoibwa, hata mishahara ya wafanyakazi wa Kampuni hiyo nayo ilifanyiwa ufisadi na kuleta usumbufu mkubwa kwa watumishi.