Mkurugenzi Mkuu wa Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa ameshiriki katika uzinduzi wa Shahada ya Uzamili katika Miliki Ubunifu katika Chuo Kikuu cha DSM.
Akizungumza katika hafla hiyo Nyaisa ameonyesha wazi kufurahishwa na uanzishwaji wa Shahada hiyo ambayo itaongeza idadi ya wataalam katika taaluma hiyo muhimu.
“Nimefurahishwa sana na uanzishwaji wa Shahada hii hivyo basi kwa atakaye fanya vizuri katika kuhitimu masomo yake akiwa na alama za juu zaidi ya wengine, BRELA itamtunza.” Nyaisa.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha DSM, Profesa William Anangisye alisema kuanzishwa kwa masomo hayo kunaendana na maono ya chuo hicho kufikia mwaka 2061.
Alisema UDSM tayari imejidhatiti kifedha na kirasilimali watu kwa ajili ya kusaidia uendeshaji wa masomo hayo kama kukarabati madarasa yatakayotumika na majengo watakayotumia kwenye kampasi ya maeneo ya Mikocheni.
Aidha Mkurugenzi Mkuu ametoa wito kwa kwa Taasisi zingine kama Chama cha Haki Miliki Tanzania (COSOTA) na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kupeleka watumishi wake kujiunga na masomo hayo kwani kwa namna moja au nyingine yatawasaidia.
Alisema kutokana na umuhimu Miliki Ubunifu ni vyema kuzingatia linapokuja suala la kutunga sera na sheria za nchi ili kulinda ubunifu na uvumbuzi.
Uzinduzi wa Shahada hiyo umefanyika chuoni hapo na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa mashrikia ya kimataifa ya haki miliki kama Shirika la Haki Miliki Afrika (ARIPO) na Shirika la Haki Miliki Duniani (WIPO).