Wadau wa mikutano ya mashauriano kati ya Serikali, wafanyabiashara na wawekezaji wameendelea kupatiwa elimu kuhusiana na majukumu ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), fursa ya wajasiriamali kupatiwa bure alama ya ubora pamoja na kuzipatia ufumbuzi wa changamoto zinawakabili.
Mikutano hiyo ya mashauriano kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa inayojumuisha Mara, Simiyu, Shinyanga na Mwanza ilianza Jumatatu, Februari 24, mwaka huu na kuhudhuriwa na mawaziri na manaibu waziri zaidi ya nane ikiwa ni mwendelezo wa mikutano iliyotangulia inayolenga kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wafanyabiasha na wawekezaji.
Mkutano wa majumuisho ya mikutano hiyo ya Kanda ya Ziwa ulifanyika jana jijini Mwanza. Katika mikutano hiyo Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Yusuf Ngenya, alitoa elimu kwa wadau hao kuhusu fursa wanazopata wafanyabiashara na wazalishaji ambao bidhaa zao zimekidhi viwango vya ubora, kuhamasisha wajasiriamali kuthibitisha ubora wa bidhaa zao bure pamoja na kuzipatia majibu changamoto wanazokumbana nazo wadau mbalimbali.
Dkt. Ngenya alitaja fursa zinazotolewa na shirika hilo kwa wajasiriamali kuwa ni pamoja kuthibitisha ubora wa bidhaa wanazozalisha bila malipo kwa miaka mitatu lengo likiwa ni kuwawezesha kupanua soko la bidhaa zao na kuwaondolea vikwazo vya kibiashara.
Alisema Serikali imeanzisha utaratibu huo ili kuwasaidia
wajasiriamali kuzalisha bidhaa zenye ubora na kupanua wigo wa masoko hayo.
Alitoa wito kwa wajasiriamali na wananchi kwa ujumla kuchangamkia fursa hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inasisitiza ujenzi wa uchumi wa viwanda.
“TBS kama taasisi wezeshi inatoa huduma ya kuthibitisha ubora wa bidhaa bure kwa wajasiriamali wadogo na wakati, lengo likiwa ni kuendeleza viwanda vya Tanzania, hivyo ni vyema wakathibitisha ubora wa bidhaa zao ili wasipate vikwazo vyovyote katika kupata soko ndani na nje ya nchi,” alisema Dkt. Ngenya.
Alisema kuwa endapo wajasiriamali hao watathibitisha bidhaa zao
itawasaidia kuzalisha bidhaa endelevu ambazo zitakuwa na soko kila
mahali ikiwemo masoko ya kikanda.
Dkt. Ngenya, alifafanua kuwa lengo la TBS ni kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara zenye tija kwa taifa, bila kuathiri taratibu na sheria za nchi.
Kutokana na umuhimu huo, alisema ndiyo maana shirika hilo limeshiriki mikutano hiyo kama taasisi wezeshi kuzipatia majibu changamoto zinazowakabili wadau, kuwaelimisha kuhusu majukumu ya shirika, maboresho kwenye masuala ya viwango na jinsi shirika lilivyoondoa baadhi ya tozo ili kurahisisha ufanyaji biashara.
Alisema Shirika litaendelea kutoa elimu ya viwango kwa Watanzania wote lengo kuu likiwa ni kuwa na uelewa wa pamoja wa masuala ya viwango na ubora wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi na zile zinaingizwa kutoka nje nchi.