Dar es Salaam Jumatano 4 March 2020….. BancABC Tanzania ambayo ni kampuni tanzu ya Atlas Mara, kwa mara nyingine imeshinda tuzo ya Visa maarufu kama “Visa E-commerce Issuing Growth Award” kutokana na huduma zake za kipekee za malipo ya mtandaoni ambazo ni salama na nafuu hapa nchini. Benki hiyo imejishindia tuzo hiyo ya Visa kutokana na matumizi ya kadi zake za Visa ambazo wateja wanatumia kulipia huduma mbali mbali kwa njia ya mtandao.
Hii inakuja ikiwa ni mara ya pili kwa benki kushinda tuzo kama hiyo. Mwaka 2016, BancABC Tanzania ilishinda tuzo hiyo kwa kuongoza kwenye matuzi ya kadi zake za Visa kutumika kwenye kulipia huduma kwa njia ya mtandao. Hii inatokana na kuwa na kadi za Visa za kipekee ambazo zina usalama wa hali ya juu kwa wateja wake.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji BancABC Tanzania Imani John alisema, ‘Tunayo Furaha kubwa kuweza kujishindia tuzo kwenye soko letu ambalo lina ushindani mkubwa sana na hii inaonyesha ni jinsi gani tumejidhatiti kuhakikisha tunawarahisishia wateja wetu kufanya miamala yao mbalimbali,’ alisema John huku akitoa shukrani za kipekee kwa wateja wa BancABC Tanzania kwa kuonyesha imani yao kwa kutumia kadi za Visa za benki hiyo kufanya malipo kwa njia ya mtandao. ‘Bila nyinyi hatungeweza kushinda tuzo hii na tunawahakikishia wateja wetu kuwa tutaendelea kutoa huduma za kipekee hili kuendelea kuweka imani kwa wateja wetu,’ John aliongeza.
Akizungumza kwenye tukio la kukabidhiwa tuzo hizo, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za kidijitali BancABC Tanzania Silas Matoi alisema ‘Ni Furaha sana kwetu kushinda tuzo hii ambayo ni mara ya pili kwetu. Shukrani za kipekee kwa wateja wetu wanaotumia kadi zetu za Visa kulipia huduma mbali mbali kwa njia ya mtandao. Matumizi ya wateja wetu wa kadi ya Visa ndio kumetufanya kushinda tuzo hii. Tunajisikia ufahari sana kuendelea kuwahudumia na tunawaahidi kuendelea kuwaletea huduma zilizo bora na nzuri zaidi,’ alisema Matoi.
Matoi aliongeza, ‘Ikiwa ni moja ya njia ya kukuza malipo yaliyo salama na rahisi kwa njia ya mtandao, mtu yeyote anaweza kumiliki kadi ya Visa hata kama hana akaunti na BancABC. Kadi ya Visa ni rahisi kuongeza fedha na inatoa wasi wasi wa kutembea na fedha taslimu wakati wa kwenda kufanya manunuzi.
Matoi alisema kuwa kadi za Visa zimeundwa kwa umakini mkubwa na mfumo salama wa chip na PIN wenye teknolojia ya hali ya juu ambayo inatumika duniani kote na hivyo kuondoa tatizo la kuibiwa. Pia kadi hii ina huduma ya kupokea ujumbe mfupi wa maneno na hivyo kumfanya mmliki kupata taarifa zote za kila muamala au malipo anayofanya kwa njia ya mtandao.
“Hakuna haja ya kuhangaika wapi unaweza kutumia kadi za Visa kwani huduma zake zinapatikana masaa 24 kwa siku saba za wiki kwenye ATM za Visa milioni 2.7 duniani kote na kwenye maduka milioni 46 ya rejareja ulimwenguni kote huku kwa Tanzania ikipatikana kwenye mashine 400 za ATM za Visa na maduka Zaidi ya 1000 yanayokubali kadi ya Visa” alisema Matoi.
Kwa upande wake, Meneja Mkazi wa kampuni ya Visa Tanzania, Bi. Olive Njoroge alisema, ‘Tunawashukuru wenzetu wa BancABC Tanzania kwa juhudi kubwa ambazo wameziweka, kwa jinsi walivyoweza kujitangaza na kuwafahamisha wateja wao kuwa unaweza kutumia kadi ya Visa kwenye kulipia bidhaa au huduma na pia kwenye kutoa fedha, lakini pia kwa kulipia huduma mbali mbali kwa njia ya mtandao. Hii ni hatua kubwa na muhimu na ndio sababu tumekuja pamoja kuwapongeza’. Alisema Njoroge huku akiongeza kuwa kadi za Visa ni salama na zinaweza kutumika popote ambapo kadi ya Visa inakubalika.