Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Samwel Sitta amesema Rais Jakaya Kikwete anaonekana kuwa tayari kuongeza muda wa bunge hilo kuendelea kujadili vifungu vya rasimu ya pili ya katiba mpya baada ya bunge la bajeti kumalizika.
Muda uliotolewa toka mwanzo ni siku 70 yani ndizo zitatumiwa na bunge maalum la katiba kujadili vifungu 17 vya hiyo rasimu lakini siku hizo 70 ndio zinakatika Aprili 28 ambapo bunge hili la katiba mpaka sasa likiwa limejadili vifungu viwili tu vya rasimu ya pili ya katiba mpya.
Namkariri Samwel Sitta akisema ‘nilionana na Rais Kikwete ili atafakari namna ya kuongeza muda wakati huohuo muelewe kwamba kule Dodoma inabidi tulipishe bunge na baraza la Wawakilishi ili bajeti ya nchi isisimame kwa sababu muda wake ni May na June’
Kuhusu maamuzi ya Samwel Sitta kukutana na viongozi wa dini askofu mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Dar es Salaam Mwadhama POLYCAP KARDINAL PENGO na Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti ISSA BIN SHABANI SIMBA, amesema ‘nilitafakari nikaona ni muhimu tunapofikia hatua flani ya mchakato huu ni vizuri kwenda kwa viongozi wetu wakuu wa Madhehebu, lengo ni kuwapasha habari za nini kinachoendelea Dodoma, wajue tumetoka wapi, sasa hivi tuko wapi na matarajio yetu ni nini’