Stori hii iliyoandikwa na BBC inasema >>> Mahakama moja nchini Misri imewahukumu watu wanne kifungo cha hadi miaka nane jela kwa kosa la vitendo vya kufanya mapenzi ya jinsia moja ambapo watu hao wanashutumiwa kuhudhuria au kupanga tafrija za vitendo vya ngono, kuvaa mavazi ya kike na kujipodoa.
Sheria ya Misri haitamki kupiga marufuku vitendo vya mapenzi ya jinsia moja lakini waendesha mashitaka wametumia sheria ya Misri inayokataza mambo fulani kufanyika hadharani kuwahukumu wapenzi hawa wa jinsia moja.
Mmoja wa watu hao amehukumiwa na mahakama ya Cairo kifungo cha miaka mitatu jela na kazi ngumu huku kikundi cha kutetea haki za binadamu chenye makao yake nchini Marekani, Human Rights First kikisema hukumu hizo zinasikitisha na kukatisha tamaa.
Kikundi hicho kimesema tangu kung’olewa madarakani Rais Mohammed Morsi mwezi Julai 2013 kumekuwa na ongezeko la watu kukamatwa kwa misingi ya jinsia zao.
Hukumu ya sasa inakumbushia kesi ya mwaka 2001 ya watu 52 kushutumiwa kwa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja na makosa mengine chini ya sheria ya Misri ambapo 23 walihukumiwa kifungo cha kufikia miaka mitano jela pamoja na kazi ngumu.
Kikundi kimoja cha kutetea haki za binadamu nchini Misri kimesema adhabu kali zilizotolewa kwa watu hao Jumatatu ni sehemu ya msako unaoendelea dhidi ya uhuru binafsi.