Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Dodoma, Sostenes Kibwengo amesema, Taasisi hiyo haitaendelea na kesi ya tuhuma za rushwa ya aliyekuwa Mbunge wa Mtera kupitia CCM, Livingstone Lusinde (Kibajaji) kutokana na kukosekana uthibitisho wowote.
Kibwengo alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma.
Kibwengo amesema kuwa hadi sasa taasisi hiyo bado haijapata uthibitisho wowote wa Mbunge huyo kuwa alitoa rushwa kwa wajumbe ili wamsaidie katika mchakato wa uchaguzi Mkuu ujao.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Lusinde amesema kuwa yeye hakutoa rushwa, bali aliyetoa taarifa hiyo alikuwa na lengo la kumchafua kisiasa.
“Pale kwangu nilikuwa na shughuli ya mjukuu wangu kwa hiyo nilikuwa na wageni wengi, mtu akatumia nafasi hiyo kunichafua na kutoa taarifa TAKUKURU kuwa nilikuwa natoa rushwa kwa wajumbe” Lusinde