Serikali inatarajia kununua ndege kubwa ya mizigo, ili kuokoa gharama na muda wa usafirishaji wa minofu ya samaki kwenda nje ya nchi, zinazowakabili wamiliki wa viwanda vya kusindika minofu hiyo Kanda ya Ziwa.
Ahadi hiyo ya Serikali imetolewa Jijini Mwanza na mkurugenzi wa Shirika la ndege Tanzania (ATCL) Ladslaus Matindi, baada ya kukamilisha ziara ya kutembelea uwanja wa ndege wa Mwanza na viwanda vya kusindika minofu ya samaki vya Nature’s Fish na Omega.
Hatua ya Serikali kutaka kununua ndege hiyo imefuata, kutokana na uhaba wa ndege za usafirishaji wa minofu ya samaki kwenda nje ya nchi, jambo linalosababisha adha ya usafiri kwa wamiliki wa viwanda vya kusindika minofu ya samaki.
Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) Mhandisi Emmanuel Koroso, amesema kutokana na tatizo hilo, Serikali imeanza kufanya mazungumzo na nchi mbalimbali za kigeni, ili kuruhusu usafirishaji wa mizigo kwa kutumia ndege zilizopo.