Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Maalim seif Sharif Hamad, amesisitiza kuwa yeye pamoja na kiongozi wa chama hicho Zitto Kabwe, hawapendi rushwa na endapo watawarudisha watoa rushwa ndani ya chama hicho watatia doa kwenye chama na nchi kwa ujumla.
Maalim ametoa kauli hiyo atika ofisi za mratibu wa chama hicho visiwani Pemba, wakati akitoa neno la shukrani kwa wananchi na wanachama waliokuja kumpokea yeye pamoja na wagombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa anatilia mkazo msimamo wake kuhusu utoaji rushwa katika msimu huu wa uchaguzi.
“Msimamo wa Mwenyekiti wa chama hiki mtoa rushwa tutamkata, sasa msije mkasema huyu ni mtu wetu, tukiwarudisha wale watoa rushwa watakuwa watoa rushwa katika chama chetu na katika nchi yetu, kiongozi wetu wa chama pamoja na Mweyekiti tunachukia rushwa” Maalim Seif
Maalim Seif amewahakikishia wananchi kuwa chama cha ACT Wazalendo, kitaheshimu maoni yao kupitia kura za maoni walizopiga katika majimbo yao huku akiwaonya wasikubali kuchanganywa na baadhi ya watu wenye tamaa zao, badala yake wasimamie lengo lao moja walilolikusudia la kuikomboa Zanzibar.
“Kwahiyo wasitokee watu wenye tamaa zao wakajaribu kuwachangayeni, wananchi tuende kwenye tulilolikusudia la kuikomboa nchi yetu, mmeshapiga kura ya maoni ,chama kitaheshimu maoni yenu” Maalim Seif