Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Magugu Ndugu Adeltus Richard Rweyendera, amefikishwa mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya shilingi 150,000.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari, Kaimu mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara Isdory Kyando amesema mtuhumiwa huyo alipokea rushwa hiyo kutoka kwa wazazi na ndugu wa washtakiwa wanne ambao walikuwa wanashtakiwa kwenye kesi namba 242/2020 ikiwa ni kishawishi cha kuwasaidia na kuwaachia washtakiwa hao kwenye kesi tajwa ambayo alikuwa anaisikiliza.
Kyando amesema awali TAKUKURU Mkoa wa Manyara ilipokea taarifa kutoka kwa wasiri ikifafanua kuwa hakimu aliomba kiasi hicho cha fedha akiwataka wazazi na ndugu wa washtakiwa hao wachangishane.
Amesema baada ya kupokea taarifa hiyo, walifanya uchunguzi wa kina na kubaini ni kweli kesi tajwa ilikuwepo katika mahakama ya mwanzo Magugu na kwamba kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na Hakimu Adeltus Richard Rweyendera huku kesi hiyo ikitajwa mara kadhaa bila kusikilizwa tangu ilipofunguliwa kwa mara ya kwanza tarehe 3/8/2020.
Uchunguzi wa TAKUKURU ulibaini kuwa wananchi hao walikamatwa kwa tuhuma za uzururaji miongoni mwao wakiwa kwenye maeneo yao ya biashara.
Hata hivyo TAKUKURU walibaini kuwa hakimu huyo aliwataka washtakiwa wote wanne wachange kiasi hicho cha fedha.
Kyando amesema baada ya kujiridhisha na ukweli huo maafisa wa Taasisi hiyo, waliandaa mtego wa rushwa na kufanikiwa kumkamata hakimu akiwa amepokea kiasi cha shilingi 150,000/ fedha ambazo aliziweka kwenye droo ya meza yake mara baada ya kuzipokea.