Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ‘Mahakama ya Mafisadi’ imewahukumu aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya (70) na wenzake wanne kulipa fidia ya Sh.Bilioni 1.5 kwa Serikali baada ya kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).
Pia imewataka kila mmoja kulipa faini ya Sh Milioni moja au kwenda jela miezi sita kwa kukiri mashitaka ya kuisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 6,000,000.
April 01, 2016 Serikali iliwapandisha kizimbani, Kitilya na wenzake ambaye ni mshindi wa taji la Miss Tanzania 1996 ambaye pia alikuwa Afisa Mwandamizi wa Benki ya Stanbic tawi la Tanzania, Shose Sinare na Sioi Solomoni na Kamishina wa Sera ya Uchunguzi wa Madeni kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Benason Shallanda (59) na Msaidizi wake Alfred Misana (50).
Awali, DPP Biswalo Mganga alidai mbele ya Jaji Immaculata Banzi kuwa alipokea barua ya washitakiwa wakiomba kuingia makubaliano ya kukiri makosa yao na kwamba baada ya majadiliano aliwafutia washitakiwa hao mashitaka 57 kati ya 58 waliyokuwa wanakabiliwa nayo.
Pia aliiomba mahakama hiyo iyapokee makubaliano hayo na kuyasajili kwa mujibu wa sheria na upande wa utetezi haukuwa na pingamizi.
Jaji Banzi alisema mahakama imeyapokea makubaliano hayo kwa mujibu wa kifungu cha 194 (D) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019 ambayo inaelekeza kila mshitakiwa ahojiwe na mahakama ichukue majibu yake.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu, DPP Mganga alidai hawana rekodi ya makosa ya nyuma ya washitakiwa hivyo,aliomba kwa kujibu wa makubaliano washitakiwa walipe Sh bilioni 1.5 kama fidia ya hasara waliyosababisha.
Jopo la mawakili wa utetezi likiongozwa na Wakili Alex Mgongolwa lilidai washitakiwa ni wakosaji wa kwanza na kwamba mshitakiwa wa kwanza (Kitilya) ni mzee ambaye anakabiliwa na maradhi mbalimbali hivyo, afya yake sio nzuri.
Pia alidai washitakiwa wote wanafamilia ikiwemo wazazi wao ambao wanawategemea katika maisha yao na kitendo cha kukaa rumande kwa miaka minne na nusu, familia hizo zilikuwa kwenye mahangaiko ya kimya kimya.
“Kukiri kwao makosa kumeokoa rasilimali fedha na muda wa mahakama lakini pia washitakiwa hawa wanatakiwa kulipa fidia katika mazingira hayo unawaingiza katika madeni ili waweze kulipa fidia. Ni rai yetu katika utoaji wa adhabu tunaomba uyazingatie utoe adhabu yenye unafuu na inayotekelezeka ili kukidhi haja ya sheria hii ambayo dhamira yake ni kupunguza mrundikano wa mahabusu,” alidai Wakili Mgongolwa.
Jaji Banzi alisema amezingatia hoja za pande zote kwamba washitakiwa ni wakosaji wa kwanza na wamekiri makosa yao kwani kwa asili ya kesi hiyo ingechukua muda mrefu.
“Pia kwa kuzingatia makubaliano waliyofikia mahakama inawahukumu kulipa faini ya Sh milioni moja au kifungo cha miezi sita jela kila mmoja. Washitakiwa wote mlipe fidia ya Sh bilioni 1.5 kwa serikali ya Tanzania kwa hasara iliyopatikana,” alifafanua Jaji Banzi.
Akisoma mashitaka mapya, Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyekomya alidai washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka ya kusababisha serikali hasara.
Alidai Mei Mosi 2012 na Juni 1, 2015 wakiwa jijini Dar es Salaam isivyo halali washitakiwa waliandaa ada ya mkopo kwa serikali ya Tanzania wa Dola za Marekani Milioni 600, 000,000 kutoka asilimia 1.4 hadi 2.4 na kusababisha serikali kupata hasara ya Dola za Marekani Milioni 6,000,00.
MABWENI YA SHULE NA VITU VYATEKETEA KWA MOTO