Baada ya mvua kunyesha kwenye jiji la Dar es salaam na kuleta maafa, vifo, hasara nyingine pamoja na foleni kubwa, Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Mohammed Mpinga ameongea na millardayo.com kuhusu foleni na barabara zilizokua zimefungwa.
Anasema >> ‘April 14 2014 jioni majira ya saa kumi na mbili na nusu pale Ruvu darajani kazi ya kufanya marekebisho imekamilika ambapo magari mengi yameanza kupita yakiwemo Malori na tayari tumekubaliana na RPC Pwani kwamba magari yanaweza kuanza kupita kama kawaida’
‘Tumesharuhusu kuendelea na safari mabasi ambayo yanataka kwenda Morogoro na safari nyingine zikiwemo za kutoka kituo kikuu cha Ubungo, vilevile kulikua na magari mengine yamekwama pale Morogoro nayo tumesha waelekeza wayaruhu kuendelea na safari ya Dar es salaam manake ni shwari’
‘Kuanzia April 15 2014 kwa barabara hiyo hali ya usafiri itarudi kama kawaida, marekebisho yamekamilika vizuri kabisa’
‘Kuhusu daraja la Visiga pale wameshakamilisha mapema kabisa na pako safi magari yanapita ila kwenye njia ya kusini mto Mzinga kwenye lile daraja lililobomoka na kunyima magari kupita, April 13 2014 walianza kuweka mawe na vifusi na jioni hii nimekwenda pale magari madogo tu ndio yanaweza kupita’
Daraja jingine linalounganisha Kongowe kwenda Kigamboni kupita kwenye mto Mkokoti, pale bado jitihada zinafanyika kuparekebisha kwa sababu gari hazipiti hususani za mafuta ambazo huwa zinafanya safari za Kigamboni lakini watu wa kawaida wanavuka kwa sababu sasa hivi hakuna maji’
‘Juhudi zinazofanyika ni kunyonya mafuta kwenye Lori lililoanguka pale ili walinyanyue na tayari taratibu za kulinyanyua zimesha anza’
Kuhusu msongamano wa magari Dar es salaam April 14 2014, hii ilisababishwa na kufungwa kwa barabara kati ya Fire na taa za Magomeni, watumiaji wote wa barabara Dar es salaam wafahamu tu kuanzia sasa njia hiyo imefunguliwa na inatumika kama kawaida, kesho (April 15 2014) wapite njia zao za kawaida kasoro ile njia ya kupita Jangwani mpaka roundabout ya Kigogo ndio bado haijafunguliwa ila Morogoro road inatumika kama kawaida’
Unapenda kila kinachonifikia kikufikie na wewe wakati huohuo? ungana na mimi kwenye twitter instagram na facebook kwa jina hilohilo la @MillardAyo