Rais wa Lebanon Michel Aoun amekiri haja ya “kuubadilisha mfumo” wa kisiasa nchini humo na kutoa wito wa kutangazwa taifa lisiloegemea dini.
Aoun, amesema hayo katika mkesha wa ziara ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Wakati huo huo vigogo wa kisiasa wa madhehebu ya Sunni akiwemo Waziri Mkuu wa zamani Saad Hariri wamempendekeza Mustapha Adib ambaye ni balozi wa Lebanon nchini Ujerumani, kuwa Waziri Mkuu mpya.
Vuguvugu la maandamano Lebanon limeipinga hatua hiyo likisema ni kinyume na mabadiliko wanayoyataka.
Ikiwa chini ya wiki nne baada ya kuzuru Beirut, kufuatia mlipuko mkubwa katika bandari ya mji huo uliowaua zaidi ya watu 180, Macron anarejea nchini humo leo kushinikiza masharti yake ya kufanywa mabadiliko.