Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amelaani kitendo cha waandamanaji wanaopinga hatua za kudhibiti kusambaa kwa maradhi ya COVID-19, kulivamia jengo la bunge na kukiita kitendo hicho cha ”aibu” akisema wametumia vibaya haki yao ya kuandamana kwa amani.
Mamia ya watu walijaribu kulivamia jengo la bunge wakati wa maandamano hayo Mjini Berlin siku ya Jumamosi.
Akizungumza na waandishi habari, Msemaji wa Merkel, Steffen Seibert amesema haki muhimu ya kuandamana kwa amani, imekiukwa na waandamanaji.
Polisi inakadiria kuwa watu 38,000 walikusanyika mjini Berlin kupinga hatua zilizowekwa kukabiliana na virusi vya corona kama vile kuvaa barakoa na kuacha nafasi kati ya mtu na mtu mwingine.
Hata hivyo, polisi waliotumia maji ya kuwasha waliwazuia waandamanaji kuingia ndani ya jengo hilo. Waziri wa Afya, Jens Spahn alitemewa mate mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akijaribu kuzungumza na waandamanaji kwenye mji wa Bergisch Gladbach.
Via: DW Swahili