Mkazi mmoja wa Kijiji cha Nyamakubiti Kata ya Majimoto Wilayani Serengeti katika Mkoa wa Mara Zablon Simioni (34) anaomba msaada kwa Serikali baada ya Baba yake mzazi kumuahidi kuwa atamuua kwa kosa la kupinga mila za ukoo zinazomtaka Mzee huyo kumuua mjukuu wake ambaye alizaliwa akiwa na ulemavu wa viungo.
Akizungumza na AyoTV ameeleza kuwa baada ya mtoto kuzaliwa 2011 katika Hospitali ya Bugando iliyopo Jijini Mwanza, aliitwa na Baba yake mzazi Kijijini kwao kwa ajili ya kupanga taratibu za ukoo na mila juu ya imani yao inayotoa adhabu ya kifo kwa mtoto anayezaliwa akiwa na ulemavu wa viungo ambapo hawakufikia muafaka.
“Baada ya kupinga wazo la baba la kumuua mtoto wangu akaanza kuleta vurugu na kunitamkia kuwa mimi ndio nitabeba adhabu ya kifo kwa sababu nimeleta mkosi kwenye ukoo na mara kwa mara amekuwa akiagiza vijana ambayo ni wadogo zangu kuniteka na kunipiga mpaka kufikia hali ya kuwa mahututi kisha kutelekezwa porini,” Zablon
Kwa upande wake Mkami Mwikabe ambaye ndiye Mama wa mtoto amesema kuwa siku chache baada ya kujifungua alianza kuona kutokuwepo kwa maelewano kati ya Baba mkwe na Mumewe kwani walinyang’anywa baadhi ya mali ikiwemo mifugo na mashamba hadi alipouliza na kujibiwa kuwa chanzo ni mtoto aliyemzaa hatakiwi katika ukoo huo kwani ni mkosi.
“Huu Mji na baadhi ya mali tulipewa na Baba mkwe sasa ameanza visa hapa vya kutufukuza na kumuomba mume wangu aniache na amuozeshe Mke mwingine bila kufanya hivyo atauliwa, naomba Serikali ya Dkt. John Magufuli inisaidie mpaka sasa hatuna pa kwenda tunaishi kwa mashaka kwani muda mwingine baba mkwe anakuja usiku akitaka kumuua Mume wangu na mie nitaenda wapi huyu Mzee anavuruga ndoa yangu,” Mkami