Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi amesema kuwa lengo la kuvitaka vyombo vya habari vya kimataifa kusajiliwa ni kutambua vyombo hivyo vinashirikiana na vyombo gani vya nchini na sio kuvizuia kuendesha vipindi vyake nchini kama inavyoripotiwa.
Kabudi ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi mteule wa Uingereza nchini Dr. David Concar na kufafanua kuwa mpaka sasa vyombo vyote vya habari vya Kimataifa vimeshatekeleza matakwa hayo ya kisheria na kupata leseni za kutangaza na kuendesha vipindi vyao.
Aidha, amefafanua kuwa wamelenga kuongeza uwazi na uwajibikaji katika fedha zinazoingia kwa asasi za kiraia (NGOs) pamoja na matumizi yake na kuwa linaendana na sheria na taratibu za kimataifa za kuzuia utakatishaji wa fedha.
Pia, wamenga kuhakikisha makundi yenye nia ovu na misimamo mikali inayokwenda kinyume na tunu za demokrasia hayatumii njia hizo kupenyeza fedha zao.
Naye Balozi Dr. David Concar amesema mazungumzo yao mbali na kulenga masuala ya kidiplomasia na maendeleo pia yalilenga kuangalia namna ya kuondoa malalamiko kutoka kwa baadhi ya NGOs na vyombo vya habari vya kimataifa kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ni uminywaji wa haki ya uhuru wa vyombo vya habari.