Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amewataka Mameneja wa Shirika la Umeme nchini TANESCO wa ngazi za Kanda, Mikoa na Wilaya kuhakikisha umeme haukatiki katika kipindi chote cha uchaguzi mkuu hususan siku ya kupiga kura.
Dkt.Kalemani ameyasema hayo baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme Megawati 48 cha Dege wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam.
“Maeneo yote kuanzia kwenye Vijiji, Kata, Wilaya na Mikoa nchi nzima umeme usikatike wakati wa uchaguzi, usikatike maeneo yote na muda wote lakini hasa hasa wakati wa kupiga kura tarehe 28, Oktoba, tunataka wananchi wapige kura kwa uhuru na uhakika.” Dkt. Kalemani ambaye alifuatana na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka na viongozi wengine wa wizara.
“Niwapongeze TANESCO na Mkandarasi kwa hatua mliyofikia ingawa Mkandarasi aliomba miezi miwili kukamilisha kazi hii mimi nimesema hapana, kwanza kazi yenyewe iliyobaki ni ndogo hivyo nimetoa mwezi mmoja kufikia Novemba ujenzi uwe umekamilika.” Dkt. Kalemani.